Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. |
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba. |
Na Dotto Mwaibale, Singida
WANANCHI wa Wilaya ya Iramba mkoani Singida, wamewataka Mkuu wa wilaya hiyo, Suleiman
Mwenda na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Michael
Matomora kujiuzulu nyadhifa zao
kufuatia kushindwa kusimamia vizuri
mapato yanayokusanywa wilayani humo.
Hayo yamebainishwa na wananchi hao leo wakati wakizungumza na mwaandishi wa
habari hii kuhusu upotevu wa zaidi ya Sh.Milioni 365 ambazo zinadaiwa kutafunwa
na watumishi na mawakala waliozikusanya kama ushuru na kodi.
Wananchi hao wameeleza kuwa Mwenda
na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Michael Matomora
wanatakiwa kuachia ngazi kwa sababu wao ndio watendaji wakuu wa wilaya hiyo
lakini wameshindwa kusimamia mapato yanayokusanywa na kuishia kuliwa na
watumishi wasio waaminifu na wakibaki wakilalamika licha ya vyombo vya dola
kama TAKUKURU na Polisi kuwepo.
"Mwenda kinachomponza ni kuwa mpole na Matomora yeye akiwa mtendaji
mkuu wa halmashauri hiyo kushindwa kuchukua hatua zozote huku akiangalia mapato
yakipotea" alisema Samuel Makala mkazi wa Misigiri.
Mkazi wa Shelui, Elinipa Shango alisema viongozi hao wapepoteza sifa na
hawana kasi anayoitaka Rais Samia Suluhu Hassan ya kukusanya mapato kwa
ajili ya kuwaletea maendeleo wananchi wa wilaya ya Iramba, mkoa na Taifa kwa
ujumla hivyo wanatakiwa kuachia ngazi.
Wananchi hao walisema kuwa mapema mwaka huu Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa
akiwa katika ziara ya kikazi wilayani humo aliagiza kurejeshwa kwa fedha hizo
lakini licha ya kauli hiyo ya kiongozi mkubwa wa nchi hakuna hatua zozote
zilichochukuliwa zaidi ya kuongezeka kwa kutafunwa fedha nyingine hadi kufikia Sh.365 huku wafujaji wa fedha
hizo wakiongezeka.
Walisema Watumishi na mawakala hao wanadaiwa kuzikusanya fedha hizo na
badala ya kuzipeleka benki kwenye akaunti za serikali waliamua kuzitafuna na
kuwa tabia hiyo imekuwa likijitokeza kila mwaka.
Kufuatia ubadhirifu huo Mkuu wa Mkoa
wa Singida,Peter Serukamba, ametoa siku saba kwa watumishi wa idara ya fedha wa
halmashauri ya wilaya hiyo kuzirejesha Sh.milioni 365 ambazo zinadaiwa
kutafunwa.
Serukamba alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na wakuu wa idara,
wahasibu na watendaji wa vijiji na kata na kueleza halmashauri hiyo ndio inayoongoza mkoani hapa
kwa watumishi wake kukusanya fedha na kuzitafuta bila kuzipeleka benki.
"Mumeenda kwenye masoko wananchi wema wamelipa ushuru na kodi lakini
mtumishi tuliokupa jukumu la kukusanya fedha baada ya kuzikusanya badala ya
kuzipeleka benki unaamua kuziweka mfukon maana yake tumekupa mtaji hili jambo
haliwezekani," alisema.
Alisema katika kipindi chake akiwa Mkuu wa Mkoa wa Singida kama kuna
mtumishi anadhani hawezi kukusanya fedha za serikali na kuzipeleka benki au halmashauri basi aache
kazi hii haraka.
Serukamba alisema katika ufisadi huu kuna mambo mawili yanajitokeza
inawekezekana kuna njama kati ya wakuu wa idara na wakusanyaji ambapo fedha
hizo zikikusanywa wanagawana na hivyo serikali kukosa mapato.
Akizungumza katika mkutano huo Mkuu
wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda, alisema tatizo hilo limekuwa sugu
kwani mwaka jana watumishi na mawakala walikuwa wanadaiwa zaidi ya Sh.millioni
200 lakini mwaka huu deni limeongezeka na kufikia zaidi ya Sh.milioni 300.
Mwenda alisema wakuu wa serikali walishafika katika wilaya ya Iramba
akiwamo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambao waliagiza fedha hizo zilizotafunwa na
watumishi zirejeshwe lakini utekelezaji wake umekuwa hafifu.
"Jambo hili limekuwa la muda mrefu, mwaka jana watendaji walikuwa
wanadaiwa zaidi ya Sh.milioni 200 pamoja na serikali kuchukua hatua kwa
watumishi waliohusika cha kushangaza ufujaji umeongezeka na kufikia Sh.milioni
300 sasa," alisema.
Alisema wananchi ni haki yao kuhoji hasa pale wanapoona fedha za serikali
zikifujwa kwani fedha hizo zaidi ya Sh.Milioni 360 ni nyingi na zingeweza
kujenga hata kituo cha afya.
Alisema hatua walioichukua ni kuwafukuza kazi watumishi 17 waliohusika na
ubadhirifu huo na Iramba kuwa ni halmashauri ya kwanza kwa kuwafukuza kazi
watumishi wengi kwa wakati mmoja.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Michael Matomora alipopigiwa simu ili kupata maoni yake kuhusu madai ya wananchi ya kuwataka wajiuzulu nyadhifa zao kwa kushindwa kudhibiti upotevu wa mapato simu yake iliita bila ya kupokelewa.
No comments:
Post a Comment