KAMATI YA YAAGIZA ULINZI WA MIUNDOMBINU - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday 16 March 2020

KAMATI YA YAAGIZA ULINZI WA MIUNDOMBINU

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso, akitoa maelekezo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, baada ya Kamati hiyo kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa barabara za juu (Interchange) katika makutano ya Ubungo, jijini Dar es Salaam


Mkandarasi kutoka Kampuni ya China Civil Engineering Construction Company Corporation (CCECC), Mhandisi Yuang, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, namna nguzo za zege zinavyotengenezwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara za juu (Interchange) katika makutano ya Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, wakisikiliza maelezo kutoka kwa Meneja mradi wa ujenzi wa barabara za juu (Interchange) katika makutano ya Ubungo Mhandisi Frank Mbilinyi, wakati kamati hiyo ilipoutembelea mradi na kukagua hatua zilizofikiwa katika ujenzi huo ambao mpaka sasa umefikia asilimia 70.


Muonekano wa ngazi ya pili iliyokamilika kujengwa katika barabara ya juu kwenye makutano ya Ubungo, jijini Dar es Salaam. Ujenzi wa barabara hizo za juu (Interchange) umefikia asilimia 70.


KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeitaka Serikali kuhakikisha inaweka ulinzi madhubuti katika miundombinu ya mradi wa barabara za juu (Interchange) katika makutano ya eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam ili idumu kwa kipindi kirefu. 

Mradi huo wenye lengo la kupunguza msongamano wa magari katika njia za barabara za Morogoro, Mandela na Sam Nujoma unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 229 na huku Serikali ikichangia fedha za fidia kwa wananchi waliopisha ujenzi wa mradi.

Ameyasema hayo Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Seleman Kakoso wakati wajumbe wa kamati hiyo walipotembelea ujenzi wa mradi huo na wajumbe hao kuridhika na hatua ya kazi zilizofikiwa kwa sasa ambao walimtaka mkandarasi kutimiza malengo kwa kadiri mkataba walivyousaini.

"Tunaipongeza Serikali,  Wizara na TANROADS kwa kazi nzuri na usimamizi kwani tumefarijika kuona miundombinu ambayo imejengwa ni mizuri na kazi iliyofikiwa ni nzuri sana hivyo tunamategemeo kwamba miundombinu hii itawanufaisha watanzania", amesema Kakoso.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, ameihakikishia kamati hiyo kuwa watasimamia utekelezaji wa miundombinu bora ya Barbara kwa kila fedha inayopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maslahi mapana ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

"Dhamira ya Serikali ni kuongeza ubora wa huduma za miundombinu ikiwemo ya barabara na pia kupunguza msongamano  katika majiji na hasa jiji la Dar es Salaam na sisi Wizara tuwahakikishie kuwa tutaendelea kutekeleza miradi kama hii ya ubungo na maeneo mbalimbali", amefafanua Naibu Waziri huyo.

Amesema kuwa watanzania wanaopita katika barabara zetu wakipoteza muda mwingi katika foleni Serikali inapata hasara  kubwa kwani uzalishaji unapungua hivyo miundombinu hii itakuwa ni mkombozi kwa Taifa kwa ujumla.

Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, ameieleza kamati hiyo kuwa ujenzi wa barabara za juu  (Interchange) katika makutano ya eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam itakuwa na uwezo wa kudumu miaka 120 ijayo na kupunguza msongamano wa magari kwa zaidi ya miaka 50 ijayo ndo hali hiyo ijirudie tena.

Aidha amewaeleza kuwa mpaka sasa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 70 na  unatarajiwa kukamilika mapema mwishoni mwa mwezi wa Julai, 2020.

"Niwatoe hofu wajumbe kuwa mradi utakamilika mapema zaidi, mkandarasi yupo mbele ya muda na changamoto ya msongamano wa magari katika makutano haya utakuwa historia", Mhandisi Mfugale.

Mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo, Mheshimiwa Munde Abdallah, amesema wamefurahi kuona mradi kama huo wa kihistoria unatekelezwa katika nchi yetu na ni sifa kwa watanzania na Serikali yetu ya Awamu ya Tano.

"Serikali imewekeza fedha nyingi katika mradi huu na ndio kazi ya fedha za Serikali ya Awamu hii chini ya Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli yenye dhamira ya dhati ya kuhakikisha maendeleo ya Tanzania yanapatikana hivyo miundombinu hii mizuri ni kivutio kwa  jiji la Dar es Salaam", amesema Mheshimiwa Munde.

No comments:

Post a Comment