Friday, 8 February 2019

WATAALAMU USTAWI WATATHMINI MAHITAJI YA KISAIKOLOJIA NJOMBE

Njombe, Tanzania.

Na Joseph Kayinga,

KUFUATIA kuongezeka kwa taarifa juu ya mauaji ya watoto mkoani Njombe, Chama cha Wataalamu wa Ustawi wa jamii nchini (TASWO), kimetuma wajumbe wake kutoka Dar es salaam kuja Njombe kwa lengo la kufanya tathmini ya mahitaji ya huduma za kisaikolojia.

Msafara huo unaongozwa na Katibu Mtendaji wa TASWO Bw. Furaha Dimitrious atakayeshirikiana na wataalamu wa Ustawi waliopo Mkoani humo ili kupata taarifa sahihi ya mahitaji ya huduma za utengamao wa akili kwa familia na wananchi waliokumbwa na matukio ya kikatili pamoja.

Ziara hiyo pia ni muendelezo wa kuiunga mkono serikali katika jitihada zake za kuwahudumia walioathiriwa kiakili na kisaikolojia kwa kuwa jukumu hilo ni moja ya wajibu wa sekta na taaluma ya ustawi wa jamii duniani.  

TASWO inalenga kubaini mahitaji ya sasa ya huduma za kisaikolojia na kiakili ambazo wataalamu wa ustawi huhusika na kusaidia kuwarejesha binadamu katika hali ya utulivu wa akili wanapofikwa ma madhara ama majanga na kupoteza wapendwa wao, waajiri wao ama vitu vinavyowatambulisha na kuwategemeza kimaisha.

Taarifa za ndani zilizopatikana kutoka TASWO zimeeleza kuwa chama kimejiandaa kutoa huduma za kisaikolojia na ambatanifu kwa kadri ya mahitaji yatakavyojitokeza kulingana na tathmini inayoendelea Njombe. Aidha chama hicho kimeanza uhamasishaji wa jamii yote ya watanzania wenye mapenzi mema kusaidia raia na hasa watoto ambao kwa namna moja wameathirika na matendo hayo ya kutisha.

Kupitia ushirikiano wa wa dhati kati ya serikali,  wataalamu na jamii madhara ya kisaikolojia na kiakili kwa watoto na familia yataweza kudhibitiwa. Imeelezwa kuwa baadhi ya athari za kisaikolojia na kiakili zinazoweza kutokana na ukatili uliofanyika ni ni pamoja na wahusika kuona maluweluwe, hofu kuu, kuhisi watu wabaya wanakufuata uendako, kutoaminiana kwa ndugu ama familia kulipizana kisasi, hasira zisizo na sababu maalum, fadhaa na sononeko. TASWO imepanga kutoa tamko lake rasmi kwa mujibu wa mahitaji yatakayobainika baada ya ziara na tathmini iliyoanza tarehe 6 Februari 2019.

Itakumbukwa kuwa ni mwezi mmoja sasa tangu kuwepo kwa habari za kutisha kutoka mkoani Njombe kupitia vyombo vya habari na mamlaka za serikali likiwemo Jeshi la polisi mkoani humo kuwa yamefanyika mauaji ya kikatili ya watoto zaidi ya ya nane mkoani humo. Taarifa zimekuwa zikieleza pia kuwa wauaji wamekuwa wakikata baadhi ya viungo kama sehemu za siri, na kuondoka navyo kabla ya kutelekeza miili ya watoto katika maeneo mbalimbali ya halmashauri za mkoa wa Njombe.

Serikali na vyombo vya dola vimeendelea na msako mkubwa kudhibiti wimbi hilo. Aidha imekemea na kuonya kuwa wahalifu  wanaohusika waache mara moja unyama huo na kwa vyovyote vile wasidhani wako salama maana watakamatwa kokote kule. 

Mauaji hayo ya kinyama hayakubaliki, hayavumiliki na wala si utamaduni wa watanzania kwani ni unyama uliokithiri dhidi ya watoto wasio na hatia. Watoto wanastahili  kulindwa, kupendwa na kuthaminiwa na si kufanyiwa ukatili wa aina wowote.

Serikali na hasa wataalamu wa Ustawi hawaamini majibu yasiyo ya kisayansi kwa tatizo kubwa kama hilo kwa kuwa haiwezekani kufuatia wimbi la mauaji hayo. Zipo taarifa zilizoandikwa na vyombo mbalimbali vya habari na zinazofuatiliwa kuwa imani za kishirikina kwa lengo la kutafuta mafanikio ya utajiri, kupandishwa vyeo kazini na kuondoa nuksi vimechangia na kuwa sababu ya mauaji ya watoto hao wasio na hatia. 

Awali serikali pamoja na wataalamu wa ustawi na watu wenye mapenzi mema walishaeleza  kuwa matendo hayo ni ukatili dhidi ya uhai wa binadamu, usiokubalika kwa kipimo chochote cha utu. Na si desturi ya jamii za kistaarabu na ya Tanzania, hivyo wahusika wanatakiwa kudhibitiwa haraka sana na vyombo husika kwa kushirikiana na wanajamii wote wa Njombe.

No comments:

Post a Comment