| Njombe, Tanzania. |
Na Joseph Kayinga,
KUFUATIA kuongezeka kwa taarifa
juu ya mauaji ya watoto mkoani Njombe, Chama cha Wataalamu wa Ustawi wa jamii
nchini (TASWO), kimetuma wajumbe wake kutoka Dar es salaam kuja Njombe kwa
lengo la kufanya tathmini ya mahitaji ya huduma za kisaikolojia.
Msafara huo unaongozwa na Katibu
Mtendaji wa TASWO Bw. Furaha Dimitrious atakayeshirikiana na wataalamu wa
Ustawi waliopo Mkoani humo ili kupata taarifa sahihi ya mahitaji ya huduma za
utengamao wa akili kwa familia na wananchi waliokumbwa na matukio ya kikatili
pamoja.
Ziara hiyo pia ni muendelezo wa kuiunga
mkono serikali katika jitihada zake za kuwahudumia walioathiriwa kiakili na
kisaikolojia kwa kuwa jukumu hilo ni moja ya wajibu wa sekta na taaluma ya ustawi
wa jamii duniani.
TASWO inalenga kubaini mahitaji
ya sasa ya huduma za kisaikolojia na kiakili ambazo wataalamu wa ustawi huhusika
na kusaidia kuwarejesha binadamu katika hali ya utulivu wa akili wanapofikwa ma
madhara ama majanga na kupoteza wapendwa wao, waajiri wao ama vitu
vinavyowatambulisha na kuwategemeza kimaisha.
Taarifa za ndani zilizopatikana
kutoka TASWO zimeeleza kuwa chama kimejiandaa kutoa huduma za kisaikolojia na
ambatanifu kwa kadri ya mahitaji yatakavyojitokeza kulingana na tathmini
inayoendelea Njombe. Aidha chama hicho kimeanza uhamasishaji wa jamii yote ya
watanzania wenye mapenzi mema kusaidia raia na hasa watoto ambao kwa namna moja
wameathirika na matendo hayo ya kutisha.
Kupitia ushirikiano wa wa dhati
kati ya serikali, wataalamu na jamii
madhara ya kisaikolojia na kiakili kwa watoto na familia yataweza kudhibitiwa. Imeelezwa
kuwa baadhi ya athari za kisaikolojia na kiakili zinazoweza kutokana na ukatili
uliofanyika ni ni pamoja na wahusika kuona maluweluwe, hofu kuu, kuhisi watu
wabaya wanakufuata uendako, kutoaminiana kwa ndugu ama familia kulipizana kisasi,
hasira zisizo na sababu maalum, fadhaa na sononeko. TASWO imepanga kutoa tamko
lake rasmi kwa mujibu wa mahitaji yatakayobainika baada ya ziara na tathmini iliyoanza
tarehe 6 Februari 2019.
Itakumbukwa
kuwa ni mwezi mmoja sasa tangu kuwepo kwa habari za kutisha kutoka mkoani
Njombe kupitia vyombo vya habari na mamlaka za serikali likiwemo Jeshi la
polisi mkoani humo kuwa yamefanyika mauaji ya kikatili ya watoto zaidi ya ya
nane mkoani humo. Taarifa zimekuwa zikieleza pia kuwa wauaji wamekuwa wakikata
baadhi ya viungo kama sehemu za siri, na kuondoka navyo kabla ya kutelekeza
miili ya watoto katika maeneo mbalimbali ya halmashauri za mkoa wa Njombe.
Serikali na
vyombo vya dola vimeendelea na msako mkubwa kudhibiti wimbi hilo. Aidha
imekemea na kuonya kuwa wahalifu
wanaohusika waache mara moja unyama huo na kwa vyovyote vile wasidhani
wako salama maana watakamatwa kokote kule.
Mauaji hayo ya kinyama hayakubaliki, hayavumiliki na wala si utamaduni wa watanzania kwani ni unyama uliokithiri dhidi ya watoto wasio na hatia. Watoto wanastahili kulindwa, kupendwa na kuthaminiwa na si kufanyiwa ukatili wa aina wowote.
Serikali na hasa wataalamu wa Ustawi hawaamini majibu yasiyo ya kisayansi kwa tatizo kubwa kama hilo kwa kuwa haiwezekani kufuatia wimbi la mauaji hayo. Zipo taarifa zilizoandikwa na vyombo mbalimbali vya habari na zinazofuatiliwa kuwa imani za kishirikina kwa lengo la kutafuta mafanikio ya utajiri, kupandishwa vyeo kazini na kuondoa nuksi vimechangia na kuwa sababu ya mauaji ya watoto hao wasio na hatia.
Awali
serikali pamoja na wataalamu wa ustawi na watu wenye mapenzi mema
walishaeleza kuwa matendo hayo ni
ukatili dhidi ya uhai wa binadamu, usiokubalika kwa kipimo chochote cha utu. Na
si desturi ya jamii za kistaarabu na ya Tanzania, hivyo wahusika wanatakiwa
kudhibitiwa haraka sana na vyombo husika kwa kushirikiana na wanajamii wote wa
Njombe.

No comments:
Post a Comment