KUISHI NI KUJIFUNZA;
Kwamba Nyerere Aliona Mbali…
Mwalimu hata mwaka 1998 aliziona nyakati hizi tunazoishi sasa na hatari zake.
Kuishi n kujifunza. Pwani wavuvi kabla ya kuingia majini kuanza safari ya kwenda kuvua, huhangaika kutafuta kama kuna sehemu ya jahazi ina tundu.
Kama wakilibaini, uliziba kwa pamba ili chombo kisije kuingia maji na wakazama baharini.
Kama nchi tumo kwenye jahazi lililotubeba sote. Tusipokuwa makini tukaziba kwa pamba tundu la kupitisha maji, basi, sote tumo hatarini kuzama.
Mwalimu aliziona hatari katika nyakati hizo na tunazoziishi sasa. Kuna ishara za misuguano baina yetu tukiwa ndani ya jahazi moja. Tumejitia upofu, hatulioni tundu lililoanza kupitisha maji chomboni.
Na katika hili la misuguano ya kiimani kwenye jamii,
Wahenga wanatuambia, kuwa kamba hukatikia pabovu.
Palipo pabovu kwenye kamba inayotuunganisha Watanzania ni kwenye hili la imani. Ndilo tundu kwenye jahazi letu.
Na siku zote, uzoefu ni mwalimu mzuri sana. Mathalan, uzoefu unatufundisha, kuwa kuwasha moto ni jambo jepesi sana, lakini, kuuzima moto, yaweza kuwa ni kazi ngumu sana.
Ona, moto ulioanza kwenye nyumba moja ya nyasi kijijini, waweza kusambaa haraka na hata kuteketeza kijiji kizima. Na tangu utotoni tumetahadharishwa hatari ya kucheza na moto.
Naam, binadamu usicheze na moto, labda iwe kwenye mazingaombwe.
Nimepata kuyanukuu maneno ya busara na hekima nyingi kutoka kwa Bi. Joy Mukanyange.
Huyu alikuwa Balozi wa zamani wa Rwanda nchini Tanzania. Mama huyu aliyatamka maneno haya miaka 26 iliyopita, takribani miezi sita kabla ya kifo cha Baba wa Taifa.
Bi. Joy Mukanyange alikiona kile ambacho Watanzania hatukukiona. Ni kama vile alikuwa mnajimu, maana, alichokisema mama yule leo ndio tunaanza kukiona. Siku ile ya Aprili 6, 1999, katika iliyokuwa Kilimanjaro Hotel, Bi Joy Mukanyanga aliyatamka haya;
” Naogopa, kwani nimeanza kuona dalili zinazojengeka za mgawanyiko wa kidini nchini Tanzania na eneo lote la Maziwa Makuu, hali ambayo inaweza kusababisha mauaji ya halaiki kama yale yaliyotokea nchini mwetu mwaka 1994.” Alisema Balozi yule wa Rwanda kabla ya kuendelea kutoa ufafanuzi wa historia ya Rwanda na matukio yaliyosababisha mauaji yale ya Wanyarwanda ya wao kwa wao.
Ndio, Bi Joy Mukanyange alikiona kile ambacho Watanzania hatukukiona.
Na tutafanya makosa makubwa, kama hata sasa, tutajifanya kuwa hatukioni kile ambacho Balozi Joy Mukanyange alikiona .
Watanzania tukubali sasa kuwa tumepatwa na bahati mbaya sana ya baadhi ya Watanzania wenzetu kuanza kupandikiza mbegu za chuki miongoni mwetu. Kuna wanaotaka tuanze kubaguana kwa misingi ya kidini.
Hili ni jambo la hatari sana. Hali tunazozipitia sasa kama taifa isiwe chachu ya kuanzisha vurugu za kijamii.
Maana, taratibu tumeanza kuizoea misamiati ya sisi na wao. Mathalan, sisi Wakristo na wao Waislamu. Sisi Wachagga na wao Wazaramo. Tunasahau, kuwa katika nchi yetu hii hakuna Sisi na Wao, kuna SISI tu.
Tutakapokumbwa na maafa ya kitaifa watakaoathirika ni SISI, hakutakuwapo na WAO.
Kuishi Ni Kujifunza.
Maggid Mjengwa.


No comments:
Post a Comment