Baadhi ya Wahariri, wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Sekta ya Uchukuzi, Bw.Gabriel Migire (Hayupo Pichani) wakati wa semina ya Wahariri iliyofanyika Jijini Dar es salaam. Katibu Mkuu-Uchukuzi Gabriel Migire akisisitiza jambo kwa Wahariri wa vyombo vya habari nchini hususani wanaporipoti kuhusu miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa nchini katika Sekta ya Uchukuzi.
KATIBU Mkuu Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Bw. Gabriel Migire amewataka wahariri wa vyombo vya habari kuongeza ufanisi katika kufanya kazi.
Akifungua semina ya Wahariri wa vyombo vya Habari nchini ambayo imeshirikisha Wahariri takribani 30 kutoka vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo televisheni, redio, magazeti na blog imelenga katika kuwawezesha Wahariri kufahamu na kuelewa zaidi kuhusu shughuli, na masuala mbalimbali ya sekta ya Uchukuzi na Reli ili waweze kutekeleza majukumu ya utoaji wa taarifa.
"Niipongeze TRC kwa hatua hii nzuri, Wahariri na waandishi wa Habari wanapaswa kuelimishwa kuhusu mambo tunayofanywa kwenye sekta ya Uchukuzi na wapeleke taarifa hizo kwa jamii kwa usahihi na ufasaha" Amesema Ndugu Migire.
Aidha, Katibu Mkuu ameongeza kuwa kutokana na umuhimu wa sekta ya Ujenzi na uchukuzi amewataka waandishi wa vyombo vya habari pamoja na Wahariri watumie weledi wao katika kupeleka taarifa kwa wananchi kwa haraka na kwa kufuata utaratibu na usahihi ili kuepusha upotoshaji.
"Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi imepewa asilimia 9.3 ya bajeti nzima ya serikali ya mwaka ambayo ni takribani tilioni 4 kila mwaka, hii inaonesha jinsi gani sekta hii ni nyeti, kwa hiyo niwaambie Wahariri mko sehemu sahihi hapa ili mpate taarifa zakuwaeleza wananchi kuhusu miradi inayotekelezwa chini ya Wizara na Shirika la Reli" Amesema Ndugu Migire.
Ameongeza kwa kusema kuwa Serikali na Viongozi wake wanahitaji vyombo vya habari katika utoaji taarifa na uhabarishaji umma ili kuleta usawa na uelewa kwa wananchi na pia kujenga uaminifu kati ya jamii na serikali.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania Ndugu Masanja Kadogosa amewaeleza Wahariri hao kuwa ujenzi wa Reli ya SGR umetokana na juhudi za Maraisi wa Jamhuri Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha uchumi wa nchi unakua na kuongeza na pia kuiunganisha Tanzania na nchi jirani haswa za Ukanda wa Magharibi mwa nchi zenye malighafi nyingi haswa za madini kama Kongo na Burundi.
No comments:
Post a Comment