KIGOMA TUMIENI LAMI KUKUZA UCHUMI, PROF MBARAWA - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Monday 9 January 2023

KIGOMA TUMIENI LAMI KUKUZA UCHUMI, PROF MBARAWA

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Thobias Andengenye wakishuhudia utiaji saini wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ya Kibondo-Mabamba Km 47.9, kati ya Mtendaji mkuu wa TANROADS na Mwakilishi wa Kampuni ya CHICO, mkoani Kigoma.

Muonekano wa barabara ya Nduta-Kibondo-Kabingo KM 62.5 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea mkoani Kigoma.

Mbunge wa Muhambwe Mhe. Florence Samizi akifurahia jambo na Mtendaji Mkuu wa TANROADS Eng. Rogatus Mativila walipokagua barabara ya Nduta-Kibondo-Kabingo KM 62.5 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea mkoani Kigoma.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila akielezea namna ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ya Kibondo-Mabamba Km 47.9. utakavyokuwa katika hafla ya utiaji saini  wa mkataba wa ujenzi huo.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila alipokagua moja ya daraja la ndani la watembea kwa miguu katika kijiji cha Makere wilayani Kasulu.

Muonekano wa barabara ya Nduta-Kibondo-Kabingo KM 62.5 ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami unaendelea mkoani Kigoma.

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa akisisitiza jambo katika hafla ya utiaji saini  wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ya Kibondo-Mabamba Km 47.9.

WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amezungumzia umuhimu wa wananchi wa mkoa wa Kigoma kutumia fursa ya ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara za lami kufanyakazi kwa bidii na kukuza uchumi.

Amesema ujenzi wa barabara za lami, meli katika ziwa Tanganyika, reli ya kisasa (SGR) na uboreshaji wa uwanja wa ndege ni dhamira ya Serikali kuunganisha mkoa huo na dunia, hivyo ni vema wananchi wakatumia fursa hizo kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kupata maendeleo. 

“Takriban KM 400 za lami zinajengwa Kigoma lengo la Serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha huduma za usafiri na uchukuzi kwa nyanja zote zinaimarika nchini kote ili kuibua fursa zote za uchumi ikiwemo kilimo na biashara”, amesisitiza Prof. Mbarawa.

Akishuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kibondo-Mabamba KM 47.9, Waziri huyo wa Ujenzi amewahakikishia wakazi wote watakaoguswa na mradi huo watalipwa fidia kwa mujibu wa sheria.

“Hatutamwonea mtu,  kwa vile fidia ni jambo la kisheria wote watakaostahili kulipwa watalipwa”, amesisitiza Prof Mbarawa.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Eng. Rogatus Mativila amesema barabara hiyo ya Kibondo-Mabamba yenye urefu wa  KM 47.9 inaunganisha mkoa wa Kigoma na mikoa ya Kagera, Geita na nchi ya Burundi kupitia Gitega hivyo kukamilika kwa ke kwa lami kutachochea biashara katika ukanda wa magharibi.

Amesema mkandarasi aliyeshinda ujenzi wa barabara hiyo ni kampuni ya CHICO kutoka China na ujenzi wake utatumia miezi 24 ambapo  takriban  shilingi bilioni 63.7 zitatumika.

Naye Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa wa miundombinu unaofanyika Kigoma na kuahidi kuhamasisha wananchi kulinda miundombinu hiyo ili idumu kwa muda uliokusudiwa na kutumia fursa ya uwepo wake kupunguza umaskini.

Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya Nduta-Kibondo-Kabingo KM 62.5 na kumtaka mkandarasi CHICO anayejenga barabara hiyo kuongeza kasi.

Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.


No comments:

Post a Comment