WAZIRI MKENDA AUNDA JOPO LA WATAALAM KWA AJILI YA KUTAFUTA FEDHA ZA KUGHARAMIA SEKTA YA KILIMO MAZAO - THE HABARII

THE HABARII

HABARI | MATUKIO | MICHEZO.


ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday, 13 May 2021

WAZIRI MKENDA AUNDA JOPO LA WATAALAM KWA AJILI YA KUTAFUTA FEDHA ZA KUGHARAMIA SEKTA YA KILIMO MAZAO

Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda akiongea na Wanahabari wa vyombo mbalimbali wakati kutangaza jopo la Wataalam kutoka Serikalini na kwenye Sekta ya Fedha katika Ofisi za Wizara ya Kilimo Jijini Dodoma leo tarehe 13 Mei, 2021.

WAZIRI wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda leo tarehe 13 Mei, 2021 ametanga jopo la Wataalam mbalimbali kutoka Serikalini na Sekta ya Fedha ili kuanza kutafuta fedha za kugharamia Sekta ya Kilimo Mazao ili kuongeza nguvu zaidi ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka ujao wa fedha wa 2021/2022.

Waziri Mkenda amesema uwekezaji katika Sekta ya Kilimo Mazao umekuwa mdogo ikilinganishwa na Sekta nyingine za uchumi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa mitaji ya uhakika, ardhi, vivutio vya uwekezaji na ukosefu wa masoko ya uhakika kwa mazao na bidhaa za kilimo. 

Waziri Mkenda amesema kwa mujibu wa taarifa za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Sekta ya Kilimo imekuwa ikipata uwekezaji mdogo ikilinganishwa na Sekta nyingine kama Viwanda, Biashara, Huduma, Mawasiliano na Ujenzi. 

“Uwekezaji kwa kipindi cha mwaka 1997 hadi 2018: Kilimo na Mifugo (14.18%), Viwanda (18.01%), Mawasiliano (15.54%), Miundombinu (12.62%).” Amekaririwa Waziri Mkenda.

Waziri Mkenda amesema baada ya kulitafakari jambo hilo kwa muda mrefu; Tarehe 22 Aprili, 2021 aliwaita Wakuu wa taasisi za fedha hususan mabenki ya biashara na kujadiliana nao ili kuja na mfumo wa uhakika wa kugharamia Sekta ya Kilimo. 

Waziri Mkenda amesema malengo ya kikao hicho ilikuwa ni kujadiliana kuhusu namna bora ya kufanya mapinduzi katika kilimo kwa kuhakikisha mitaji inapatikana kwa Wakulima na Wadau katika kilimo; Itakayowawezesha kuwekeza katika mnyororo wa thamani wa  mazao mbalimbali ya kilimo ikiwemo kupata pembejeo, uanzishaji na uendelezaji wa viwanda vya kuongeza thamani ya mazao na uhakika wa kupata masoko ya mazao wanayozalisha.

Waziri Mkenda ameongeza kuwa katika kikao chake hicho na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Fedha aliwaambia kuwa Wizara imejiwekea vipaumbele vichache kitika Bajeti yake ijayo kwa mwaka 2021/2022; Vipaumbele hivyo ni pamoja na utafiti kwenye mbegu bora na mbinu bora za kilimo; Huduma za ugani ili kuongeza tija ambayo ni jawabu la kuzalisha mazao kwa wingi na yenye ubora ndani ya eneo dogo;

“Kipaumbele kingine ni kuongeza uzalishaji wa mbegu bora; Bila mbegu bora hakuna tija ya uzalishaji na kukibadilisha kilimo nchini; Masoko ya ndani na nje ya nchini, ambapo mkazo utawekwa katika kuzalisha kwa kiasi na ubora unaohitajika katika soko, kuhamasisha kilimo cha mkataba, mikataba baina ya Tanzania na nchi nyingine.” Amesisitiza Waziri Mkenda.

Kipaumbele kingine ni ambacho Waziri Mkenda amekitaja ni umwagiliaji na ugharamiaji wa kilimo (Agriculture financing) ili kuweza kufanya mapinduzi ya kilimo yenye tija.

Waziri Mkenda amesema ili kufanikisha jambo hilo Wizara ya Kilimo imeunda timu ya Wataalam kutoka Serikalini na kwenye Sekta ya Fedha na Mitaji na kuongeza kuwa itakuwa na Wajumbe tisa huku ikiongozwa na Mwenyekiti na Katibu wa Jopo.

Waziri Mkenda amemtaja Naibu Waziri Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) kuwa Mwenyekiti huku Katibu wa Jopo hilo ni Prof. Siza Tumbo, Naibu Katibu Mkuu Kilimo. 

Wajumbe wa Jopo hilo ni pamoja na Abdumajid Nsekela, Mkurugenzi Mtendaji Benki ya CRDB, (Mjumbe) Ruth Zaipuna, Mkurugenzi Mtendaji, Benki ya NMB (Mjumbe), Japhet Justine, Mkurugenzi Mtendaji, Benki ya TADB (Mjumbe), Theobald Sabi, Mkurugenzi Mtendaji, Benki ya NBC (Mjumbe), Anna Shanalingigwa, Mkurugenzi Mtendaji, PASS Trust (Mjumbe), Sabasaba Moshingi, Afisa Mtendaji Mkuu, TPB (Mjumbe), Charles Itembe, Mkurugenzi Mtendaji, Benki ya Azania (Mjumbe), Charles Singili, Mkurugenzi Mtendaji, TIB-DFI (Mjumbe) na Dkt. Benson Ndiege, Mrajis wa Vyama vya Ushirika, TCDC (Mjumbe).

Kazi moja wapo ambayo Waziri Mkenda amesema timu hii itaanza nayo ni suala la changamoto ya mafuta ya kula ambayo Serikali inatumia karibu nusu trilioni kuagiza mafuta ya kula kutoka nje ya nchi. 

“Watakuja na mapendekezo ya namna ya kupunguza gharama za mitaji na upatikanaji wake utakaowezesha kuwekeza katika uzalishaji wa mbegu za mafuta ya kula na kuboresha viwanda vya usindikaji vilivyopo.” Amekaririwa Waziri Mkenda.


No comments:

Post a Comment