Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Mhe. Dk. Sira Ubwa Mamboya (mbele) akitembelea miundombinu na mitambo ya mawasiliano inayosimamiwa na TTCL Corporation. Wengine ni maofisa kutoka TTCL Corporation, na Wizara ya Mawasiliano Zanzibar.
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar Mhe. Dkt. Sira Ubwa Mamboya, amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na
Shirika lsa Mawasiliano Tanzania( TTCL Corporation) katika kutoa huduma bora za
Mawasiliano na usimamizi wa Miundombinu ya Kimkakati ya Mawasiliano Nchini.
Mhe Waziri Dkt. Sira Ubwa Mamboya,ametoa pongezi hizo Jijini Dar Es Salaam
mara baada ya ziara yake katika Shirika la Mawasiliano Tanzania, kutembelea
Miundombinu na Mitambo ya Mawasiliano inayosimamiwa na TTCL Corporation.
Katika salamu zake, Mhe Waziri amepongeza utendaji wa TTCL mpya ambayo
inafanya juhudi kubwa za kuliimarisha Shirika na huduma zake na kuonesha
kufurahishwa na utaratibu wa Shirika hilo kutoa ajira kwa kuzingatia pande zote
za Muungano hali inayoimarisha udugu na uhusiano mwema.
Akizungumza katika salamu za kumkaribisha Mhe. Waziri, Mkurugenzi Mkuu wa
TTCL Corporation Bw Waziri Kindamba amewashukuru viongozi Wakuu wa SMZ kwa
uongozi wao thabiti unaodumisha Muungano na kustawisha ushirikiano unaoiwezesha
TTCL Corporation kutimiza vyema majukumu yake katika Ofisi zake zote Tanzania
Visiwani ambapo inaihudumia Serikali, Taasisi za Umma na Sekta binafsi.
“Tunapopata ugeni kama huu, tunafarijika sana kwani kupitia tukio
hili, uhusiano mwema wa kindugu baina ya pande mbili za Muungano unaimarishwa,
Aidha, tunabadilishana ujuzi na uzoefu pamoja na kujenga mtazamo wa pamoja wa
namna bora zaidi ya kuwahudumia Wananchi wetu” amesema Kindamba.
Shirika la Mawasiliano
Tanzania-TTCL Corporation lilizaliwa tarehe 01 Februari 2018, kwa Sheria ya
Shirika la Mawasiliano Tanzania Na. 12 ya mwaka 2017. Kuundwa upya kwa Shirika
hili la TTCL Corporation ni matokeo ya kukamilika kwa mchakato wa kutunga
sheria uliopitia katika hatua zake zote ikiwemo kuridhiwa na Bunge na hatimaye
kupata idhini ya Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 28 Novemba, 2017.
Huduma za
mkongo wa Taifa wa Mawasiliano zinazosimamiwa na kuendeshwa na TTCL
zimeiwezesha Tanzania kuwa Nchi ya kupigiwa mfano katika Ukanda wa kiuchumi wa
Nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara kutokana na kuwa na mfumo mzuri zaidi
kukusanya kodi kwa kutumia mfumo maalumu wa kielektroniki wa Serikali
ujulikanao kama GePG.
|
No comments:
Post a Comment