WAKILI MSANDO AKOSHWA NA HUDUMA ZA MUHIMBILI MLOGANZILA, AWAPA KONGOLE WATAALAM - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Friday, 19 September 2025

WAKILI MSANDO AKOSHWA NA HUDUMA ZA MUHIMBILI MLOGANZILA, AWAPA KONGOLE WATAALAM

MKUU wa Wilaya ya Ubungo Wakili Albert Msando ameushukuru na kuupongeza Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila kwa namna ambayo umeendelea kusimamia ubora wa huduma na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kibingwa na kibingwa bobezi bila kujali hali zao za kipato.

Wakili Msando ameyasema hayo wakati aliposhiriki uzinduzi wa Kliniki Maalumu (Premier Clinic) ambayo huduma zake zina hadhi na ubora wa kimataifa, na kuweka historia ya kuwa miongoni mwa hospitali chache ambazo zina kiliniki maalumu nchini.

Wakili Msando ameongeza kuwa pamoja na hospitali hiyo kuwa na miundombinu, vifaa tiba vya kisasa na wataalam wenye weledi wa hali ya juu nchini haibagui wananchi kwani inapokea na kuhudumia wananchi wote hata wa kipato cha chini.

“Niwapongeze sana, ninyi mmeitikia wito wa Serikali wa kuhakikisha kila Mwananchi anapata huduma zinazostahili, mmeonesha utu, upendo, kujali na uzalendo wa hali ya juu, wananchi wamekuwa wakitoa ushuhuda wa huduma zenu, haya yote yanatokana na uongozi thabiti na imara mliounesha” amebainisha Wakili Msando

Kuanzishwa kwa kiliniki maalumu kunaenda sambasamba na uwepo wa wodi za watu mashuhuri ambazo zinalaza wagonjwa mbalimbali wa ndani na nje ya nchi, kitendo ambacho mmeendelea kuchochea tiba utalii nchini.

Kliniki hiyo imezinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambapo viongozi mbalimbali wameshiriki, viongozi kutoka Wizara ya Afya, wakuu wa taasisi chini ya Wizara ya Afya, wadau mbalimbali pamoja na wataalam wa hospitali hiyo.

https://www.instagram.com/p/DOwFy2AjMvZ/?igsh=MWNlN3gybGxidDF0dw== 

No comments:

Post a Comment