Na Mwandishi Wetu, Dar
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imetoa utabiri wa mwelekeo wa mvua za msimu wa vulu kwa kipindi cha kuanzia Mwezi Oktoba hadi Disemba 2025, ambao kiujumla unaonesha mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya Wastani, huku maeneo mengi yakitawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha.
Akitoa utabiri huo leo jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a amebainisha kuwa, mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Oktoba, 2025 katika maeneo ya mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Mara na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
Amesema mvua hizo pia zitasambaa katika maeneo ya pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba 2025, kabla ya kukoma kwenye mwezi Januari, 2026.
Aidha, Dk. Chang'a ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), amebainisha uwepo wa ongezeko la mvua kidogo tena ifikapo mwezi Desemba, 2025 katika utabiri huo.
"Mvua zinatarajiwa kuwa za Wastani hadi Chini ya Wastani katika maeneo mengi na kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha hususan katika maeneo ya pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki," alisema Dkt. Chang’a.
Pamoja na hayo, ameeleza kutakuwa na vipindi vya joto kali kuliko kawaida katika msimu huu wa Vuli utakaoweza kuchangia uwepo wa upungufu wa unyevunyevu katika udongo katika maeneo mengi na hivyo kuathiri shughuli za kilimo.
"Msimu unatarajiwa kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha hususan katika maeneo ya pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki. Aidha, ongezeko la mvua linatarajiwa kujitokeza mwezi Desemba, 2025 katika maeneo mengi," alisisitiza katika utabiri huo.
Hata hivyo, ameshauri wataalam wa sekta za Kilimo, afya, Mifugo na Uvuvi, Utalii na Wanyamapori, Usafiri na Usafirishaji, Nishati, Maji na Madini kuchukua hatua kulingana na mabadiliko hayo ya hali ya hewa ili kupunguza athari ambazo zinaweza kujitokeza.
TMA itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mirejesho ya mwelekeo wa mvua nchini kadri inavyohitajika. Aidha, wadau wanashauriwa kuwasiliana na Mamlaka ili kupata taarifa mahsusi za utabiri wa msimu ili kukidhi mahitaji maalum katika sekta zao.




No comments:
Post a Comment