MASWALI NA MAJIBU KUHUSU UKAGUZI WA ASKARI BARABARANI - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Sunday 8 August 2021

MASWALI NA MAJIBU KUHUSU UKAGUZI WA ASKARI BARABARANI

 


MASWALI NA MAJIBU KUHUSU UKAGUZI WA ASKARI BARABARANI

1. Je, askari wa aina gani anaruhusiwa kusimamisha na kukagua  magari barabarani? 

Kwa mujibu wa kif.81 cha Sheria ya Usalama Barabarani (RTA), askari yeyote wa Polisi anaruhusiwa kusimamisha na kukagua gari barabarani. Huu ni ukaguzi wa kawaida kabisa haujalishi dereva ana kosa au hana kosa. Tunasema askari yeyote kwa sababu hakuna sehemu yoyote katika sheria palipoandikwa traffic Police, maneno yaliyopo ni Police Officer yakimaanisha afisa wa Polisi. 


2. Je, askari akisimamisha gari anakagua vitu gani?

Ukaguzi wa askari umegawanyika katika mafungu 3:

(a) Ukaguzi wa dereva.

Hapa askari anajielekeza katika kumkagua dereva kama dereva ili kujiridhisha iwapo dereva huyo ni halali au leseni aliyonayo ni halali. Kutimiza hili askari atamkata dereva atoe leseni yake ili aikague. Mamlaka ya kutaka leseni ili aikague anayo askari kwa mujibu wa kif.77 cha Sheria. 


(b) Ukaguzi wa gari

Baada ya kujiridhisha juu ya  uhalali wa dereva, kinachofuata ni ukaguzi wa gari ili kuona kama linafaa kwa matumizi barabarani (roadworthiness) kwa mujibu wa kif. 39(1)(a) na  (b) cha Sheria. Kwa askari asiye mkaguzi wa magari huyu atajielekeza katika ubovu unaoonekana dhahiri. Mfano kutokuwa na mkanda. 


(c) ukaguzi wa masuala mengine yanayoongozwa na sheria nyingine kama vile Sheria ya Usafirishaji,  Bima, Jinai nk.

Hapa askari anaweza kukagua na akakutana na kitu kisichohusiana na sheria ya usalama baraharani lakini ni kosa, bado akaweza kumchukulia hatua dereva husika. Mamlaka haya ni kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi. 


3. Je, ni halali askari kusimamisha gari na kudai leseni kwa dereva bila kumuelekeza kosa?

Ndiyo ni halali. Ni halali kwa kuwa ukaguzi wa leseni ni jambo linalojitegemea kwa mujibu wa kif.77. Askari anaweza akamsimaisha dereva akakagua leseni tu na kumwacha dereva aende. Na sio lazima akichukua leseni aandike kosa. Anataka tu kumtambua dereva na kujiridhisha na uhalali wake. 


Hata hivyo, ieleweke kwamba hata askari akimsimamisha dereva kwa kosa fulani lazima atataka leseni kwanza. Hii ni kwa sababu leseni ndio yenye taarifa za msingi za dereva. 


4. Je, ni halali askari kuchukua tu leseni ya dereva na kumwandikia kosa bila kumweleza kosa?

Si halali kufanya hivyo. Askari anayemsimamisha dereva kwa sababu ya kosa fulani au akagundua kosa baada ya ukaguzi, ni wajibu wake kumweleza dereva dereva kosa lake ili dereva apate kukubali au kukataa kosa. 


5. Je, askari ana haki ya kuishika leseni ya dereva na kuikagua au aione tu kwa mbali?

Kwa mujibu wa kif.77 askari anatakiwa achukue leseni na kuikagua. Kuikagua ni kuiangalia kama picha inaendana na dereva, madaraja yaliyoandikwa yanaendana na gari, leseni haijaishi muda wake, nk. Ili afanye yote haya lazima aishike. Isitoshe leseni ni mali ya serikali na ndo maana ikifutwa au kufungiwa inarudishwa. 


Hata hivyo si halali kwa askari kubaki na leseni ya dereva bila sababu za msingi. Na ndio maana leseni ya dereva ikichukuliwa kuna form maalumu ya polisi ambayo dereva anapaswa kujaziwa kama ushahidi kuwa leseni yake imechukuliwa. 


Ni imani yetu makala hii imekuongezea maarifa 


RSAadmin1

RSA Tanzania

Usalama Barabarani ni Jukumu Letu sote.

No comments:

Post a Comment