TMA YATOA UTABIRI WA MVUA ZA MSIMU NOVEMBA, 2019 HADI APRILI, 2020 - THE HABARII

ASAS GROUP

Habari Mpya


Thursday 10 October 2019

TMA YATOA UTABIRI WA MVUA ZA MSIMU NOVEMBA, 2019 HADI APRILI, 2020

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA Dk. Agnes Kijazi akizungumza na waandishi wa habari alipokuwa akitoa utabiri wa hali ya hewa kuhusu mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka. Kulia kwake ni Meneja Kituo Kikuu cha Utabiri TMA, Bw. Samwel Mbuya na kushoto ni MKurugenzi wa Huduma za Utabiri Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA, Dk. Hamza Kabelwa.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa TMA Dk. Agnes Kijazi akizungumza na waandishi wa habari alipokuwa akitoa utabiri wa hali ya hewa kuhusu mwelekeo wa mvua za Msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka. Mkutano huo umefanyika Makao Makuu ya TMA, Jengo la Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam.

Na Joachim Mushi, Dar 

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa mwelekeo wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka.

Akizungumza katika mkutano na wanahabari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi amesema mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa, Ruvuma, kusini mwa mkoa wa Morogoro, Lindi na Mtwara inatarajia kuwa na mvua za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi, huku kwa maeneo yaliyosalia katika Mikoa ya Kigoma, Katavi na Rukwa yakitarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

Hata hivyo, alisema mvua nyingi inatarajiwa kunyesha katika nusu ya kwanza ya msimu wa NDJFMA 2019/20 kutokana na uwezekano wa uwepo wa upepo kuvuma kutoka magharibi, huku kipindi cha nusu ya pili cha msimu, mvua zikitegemewa kupungua katika baadhi ya maeneo kutokana na joto la bahari.

"..Mvua za Msimu ni mahususi katika maeneo ya magharibi mwa nchi, kanda ya kati, nyanda za juu kusini magharibi, kusini mwa nchi, ukanda wa pwani ya kusini pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro. Maeneo haya yanapata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka, unaoanza mwezi Novemba hadi Aprili ya mwaka unaofuata," alisema Mkurugenzi Mkuu Kijazi.

Aliongeza kuwa kwa mikoa ya Kigoma, Tabora na Katavi yanatarajiwa kuwa na mvua za juu ya wastani hadi wastani katika mkoa wa Tabora, huku mvua za wastani hadi juu ya wastani zikitarajiwa katika mikoa ya Kigoma na Katavi.

"...Mvua hizi zinatarajiwa kuanza katika wiki ya nne ya mwezi Oktoba, 2019 katika mkoa wa Kigoma na kusambaa katika mikoa ya Katavi na Tabora katika wiki ya kwanza ya mwezi Novemba, 2019. Mvua hizo zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya tatu na wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2020," alisisitiza Dkt. Agnes Kijazi.

Kwa mikoa ya Singida na Dodoma; alibainisha mvua katika maeneo haya zinataraji kuanza katika wiki ya kwanza hadi wiki ya pili ya mwezi Novemba, 2019, huku yakiwa na mvua za juu ya wastani hadi wastani, ambazo zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya pili na wiki ya tatu ya mwezi Aprili, 2020. 

"Nyanda za juu kusini magharibi na maeneo ya kusini mwa nchi yaani mikoa ya Rukwa, Songwe,  Mbeya, Iringa, Njombe, Ruvuma pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro mvua zitaanza kati ya wiki ya kwanza na wiki ya pili ya mwezi Novemba, 2019 na zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi."

Hata hivyo, amesema katika maeneo machache ya magharibi mwa mkoa wa Ruvuma mvua zinatarajiwa kuwa za wastani na zitaisha kati ya wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2020 na wiki ya kwanza ya mwezi Mei, 2020.

Aliongeza kuwa kwa mikoa ya Lindi na Mtwara, mvua zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya kwanza na wiki ya pili ya mwezi Novemba, 2019 na zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mengi, huku zikitazamiwa kumalizika wiki ya kwanza ya mwezi Mei, 2020.



No comments:

Post a Comment